Proverbs 25

Mithali Zaidi Za Sulemani

1 aHizi ni mithali zaidi za Sulemani, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:
2 bNi Utukufu wa Mungu kuficha jambo,
bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.


3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini,
ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.


4 cOndoa takataka kwenye madini ya fedha,
nako ndani yake kutatokea chombo
cha mfua fedha.

5 dOndoa waovu mbele ya mfalme,
nacho kiti chake cha enzi
kitaimarishwa kwa njia ya haki.


6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme,
wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;

7 eni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,”
kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu.

Kile ulichokiona kwa macho yako

8 fusiharakishe kukipeleka mahakamani,
maana utafanya nini mwishoni
kama jirani yako atakuaibisha?


9 gKama ukifanya shauri na jirani yako,
usisaliti siri ya mtu mwingine,

10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha
na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.


11 hNeno lisemwalo kwa wakati ufaao
ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu
yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.


12 iKama vile kipuli cha dhahabu
au pambo la dhahabu safi,
ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima
kwa sikio lisikilizalo.


13 jKama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno
ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao,
huburudisha roho za bwana zake.


14 kKama vile mawingu na upepo pasipo mvua
ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.


15 lKwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa,
nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.


16 mUkipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha,
ukila zaidi, utatapika.

17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache,
ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.


18 nKama vile rungu au upanga au mshale mkali
ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.


19 oKama vile jino bovu au mguu uliolemaa,
ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.


20 pKama vile avuaye mavazi siku ya baridi,
au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi,
ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.


21 qKama adui yako ana njaa, mpe chakula ale;
kama ana kiu, mpe maji anywe.

22 rKwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake,
naye Bwana atakupa thawabu.


23 sKama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua,
ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.


24 tNi afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,
kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.


25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka
ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.


26 uKama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au
kisima kilichotiwa taka
ndivyo alivyo mtu mwenye haki
akishiriki na waovu.


27 vSi vyema kula asali nyingi sana,
wala si heshima
kujitafutia heshima yako mwenyewe.


28 wKama vile mji ambao kuta zake zimebomoka
ndivyo alivyo mtu
ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.
Copyright information for SwhKC